Sera ya Faragha ya Spotify

Itaanza kutumika 10 Oktoba 2024

1. Kuhusu Sera hii

2. Vidhibiti na haki za data yako ya binafsi

3. Data binafsi tunayokusanya kukuhusu

4. Kusudi letu la kutumia data yako ya binafsi

5. Kushiriki data yako ya binafsi

6. Uhifadhi wa data

7. Kuhamishia nchi zingine

8. Kutunza usalama wa data yako ya binafsi

9. Watoto

10. Mabadiliko ya Sera hii

11. Jinsi ya kuwasiliana nasi

1. Kuhusu Sera hii

Sera hii inafafanua jinsi tunavyoshughulikia data yako ya binafsi katika Spotify AB.

Inatumika kwenye matumizi yako ya:

  • huduma zote za utiririshaji za Spotify kama mtumiaji. Kwa mfano, hii ni pamoja na:
    • matumizi yako ya Spotify kwenye kifaa chochote
    • uwekeaji mapendeleo hali yako ya utumiaji
    • miundombinu inayohitajika ili kutoa huduma zetu
    • kuunganisha akaunti yako ya Spotify na programu nyingine
    • machaguo yetu mbili ya kutiririsha bure au kwa malipo (kila moja inaitwa 'Chaguo la Huduma')
  • huduma nyingine za Spotify zinazojumuisha kiungo kinachoelekeza kwenye Sera hii ya Faragha. Hizi ni pamoja na tovuti za Spotify, Huduma kwa Wateja na Tovuti ya Jumuiya

Kuanzia sasa, tutaita huduma hizi kwa pamoja 'Huduma ya Spotify'.

Mara kwa mara, tunaweza kubuni au kutambulisha huduma za ziada. Zitazingatia pia Sera hii, isipokuwa tubainishe vinginevyo tunapozitambulisha.

Sera hii si...

  • Masharti ya Kutumia Spotify, ambayo ni hati tofauti. Masharti ya Kutumia yanabainisha mkataba wa kisheria kati yako na Spotify kwa matumizi ya Huduma ya Spotify. Yanabainisha pia kanuni za Spotify na haki zako za mtumiaji
  • kuhusu matumizi yako ya huduma nyingine za Spotify ambazo zina sera yake ya faragha. Huduma nyingine za Spotify ni pamoja na Anchor, Soundtrap, Megaphone na programu ya Spotify Live

Nyenzo na mipangilio mingine

Maelezo muhimu kuhusu data yako binafsi yanapatikana hapa katika Sera hii. Hata hivyo, tunapendekeza upitie vidhibiti na nyenzo zetu nyingine za faragha:

  • Kituo cha Faragha: Kituo kinachofaa watumiaji kilicho na muhtasari wa mada muhimu.
  • Faragha ya Akaunti: Dhibiti uchakataji wa data fulani ya binafsi, ikiwa ni pamoja na matangazo ya kulenga.
  • Mipangilio ya Arifa: Chagua mawasiliano ya mauzo unayopokea kutoka Spotify.
  • Mipangilio (inayopatikana kwenye matoleo ya Kompyuta na Vifaa vya mkononi ya Spotify): Dhibiti vipengele fulani vya Huduma ya Spotify kama vile 'Maudhui Dhahiri' au 'Ya Kijamii'. Kwenye mipangilio ya 'Kijamii', unaweza:
    • kuanzisha kipindi cha Faragha
    • kuchagua iwapo utashiriki unachosikiliza kwenye Spotify na wanaokufuatilia
    • kuchagua iwapo utaonyesha wasanii uliocheza kazi zao hivi karibuni kwenye wasifu wako wa umma

Kwenye mipangilio ya 'Maudhui Dhahiri' unaweza kudhibiti iwapo maudhui yaliyokadiriwa kuwa ni dhahiri yanaweza kuchezwa kwenye akaunti yako ya Spotify.

  • Sera ya Vidakuzi: Maelezo kuhusu jinsi ya kutumia vidakuzi na jinsi ya kudhibiti mapendeleo yako ya vidakuzi. Vidakuzi ni faili zinazohifadhiwa kwenye simu, tableti au kompyuta yako unapotembelea tovuti.

2. Vidhibiti na haki za data yako ya binafsi

Sheria nyingi za faragha huwapa watu haki juu ya data yao ya binafsi. Sheria hizi ni pamoja na Kanuni ya Jumla ya Ulinzi wa Data, au 'GDPR'.

Baadhi ya haki zinatumika Spotify inapotumia 'misingi fulani ya kisheria' kuchakata data yako. Tunafafanua kila misingi ya kisheria na wakati ambapo Spotify inatumia kila mojawapo, katika Sehemu ya 4 'Kusudi letu la kutumia data yako ya binafsi'.

Jedwali hapa chini linafafanua:

  • haki zako
  • hali zinapotumika (kama vile kigezo cha kisheria kinachohitajika)
  • jinsi ya kuzitumia
Ni haki yako...
Vipi?

Pata taarifa

Pata taarifa kuhusu data ya binafsi tunayoichakata kukuhusu na jinsi tunavyoichakata.

Tunakupa taarifa:

  • kupitia Sera hii ya Faragha
  • kupitia maelezo unayopewa unapotumia Huduma ya Spotify
  • kwa kujibu maswali na maombi mahususi unapowasiliana nasi

Idhini ya kufikia

Omba idhini ya kufikia data ya binafsi tunayochakata kukuhusu.

Ili uombe nakala ya data yako ya binafsi kutoka Spotify, unaweza:

Unapopakua data yako utapokea taarifa kuhusu data yako ambayo Spotify inapaswa kukupa kwa mujibu wa Kifungu cha 15 cha GDPR. Ikiwa unahitaji maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyoshughulikia data yako ya binafsi, unaweza kuwasiliana nasi.

Urekebishaji

Tuma ombi ili turekebishe au tusasishe data yako ya binafsi pale ambapo si sahihi au haijakamilika.

Unaweza kubadilisha Data yako ya Mtumiaji chini ya ‘Badilisha wasifu’ katika akaunti yako au kwa kuwasiliana nasi.

Kufuta

Tuma ombi ili tufute baadhi ya data yako ya binafsi.

Kwa mfano, unaweza kutuomba tufute data yako ya binafsi:

  • ambayo hatuihitaji tena kwa ajili ya kusudi lililotufanya tuikusanye
  • tunayochakata kuligana na misingi ya sheria ya idhini, na uondoe idhini yako
  • unapopinga (angalia sehemu ya 'Pingamizi' hapa chini) na
    • unapotoa pingamizi la haki, au
    • unapopinga matangazo ya moja kwa moja

Kuna hali ambapo Spotify haiwezi kufuta data yako, kwa mfano wakati:

  • bado tunahitaji kuchakata data kwa ajili ya kusudi lililotufanya tuikusanye
  • hitaji la Spotify la kutumia data linapewa kipaumbele ikilinganishwa na hitaji lako la kuifuta. Kwa mfano, pale tunapohitaji data kwa ajili ya kulinda huduma zetu dhidi ya ulaghai
  • Spotify ina wajibu wa kisheria wa kuhifadhi data, au
  • Spotify inahitaji data ili kuanzisha, kutekeleza au kutetea madai ya kisheria. Kwa mfano, ikiwa kuna tatizo ambalo halijatatuliwa linalohusiana na akaunti yako

Kuna njia kadhaa unazoweza kutumia kufuta data ya binafsi kutoka Spotify:

  • ili uondoe maudhui ya sauti kwenye wasifu wako teua maudhui husika kisha uchague kuyaondoa. Kwa mfano, unaweza kuondoa orodha za kucheza kwenye wasifu wako, au kuondoa wimbo kwenye orodha yako ya kucheza
  • ili uombe tufute data yako ya binafsi kwenye Spotify, fuata hatua zilizo kwenye ukurasa wetu wa usaidizi. Data hii ni pamoja na Data ya Mtumiaji, Data ya Matumizi na data nyingine iliyoorodheshwa katika Sehemu ya 3 ‘Data ya binafsi tunayokusanya kukuhusu'
  • unaweza pia kuwasiliana nasi ili uombe ifutwe

Vikwazo

Tuma ombi ili tuache kuchakata baadhi au data yako yote ya binafsi.

Unaweza kufanya hivi ikiwa:

  • data yako ya binafsi si sahihi
  • uchakataji wetu ni kinyume cha sheria
  • hatuhitaji maelezo yako kwa kusudi mahususi, au
  • unapinga uchakataji wetu na tunatathmini ombi lako la pingamizi. Angalia sehemu ya 'Pingamizi' hapa chini

Unaweza kuomba kuwa tusitishe uchakatakaji huu kwa muda au kabisa.

Unaweza kutekeleza haki yako ya kuweka vikwazo kwa kuwasiliana nasi.

Pingamizi

Weka pingamizi ili tuache kuchakata data yako ya binafsi.

Unaweza kufanya hivi ikiwa:

  • Spotify inachakata data yako ya binafsi kwa misingi ya kisheria ya maslahi halali, au
  • Spotify inachakata data yako ya binafsi kwa matangazo yanayolenga

Ili utekeleze haki yako ya kupinga, unaweza:

  • kutumia vidhibiti kwenye Huduma ya Spotify kuzima au kurekebisha baadhi ya vipengele vinavyochakata data yako ya binafsi. Angalia mwisho wa sehemu hii ili uone jinsi ya kudhibiti matangazo yanayolenga
  • wasiliana nasi

Uhamishaji wa data

Tuma ombi la kupewa nakala ya data yako ya binafsi katika muundo wa kielektroniki na haki ya kutuma data hiyo ya binafsi kwa matumizi katika huduma ya watoaji wengine.

Unaweza kutuomba tutume data yako wakati tunachakata data yako ya binafsi kwa misingi ya kisheria ya idhini au utendaji wa mkataba. Hata hivyo Spotify bado itajaribu kutii ombi lolote kwa kadri inavyowezekana.

Kwa maelezo kuhusu namna ya kutekeleza haki ya kuhamisha, angalia 'Idhini ya kufikia' hapo juu.

Usiathiriwe na maamuzi yanayofanywa kiotomatiki

Usiathiriwe na maamuzi yanayofanywa kiotomatiki pekee (maamuzi yasiyo na mchango wa mtu), ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji kulingana na vigezo fulani, ambapo maamuzi yatakuwa na athari ya kisheria kwako au yawe na athari nyingine kubwa kama hiyo.

Spotify haitekelezi aina hii ya maamuzi ya kiotomatiki kwenye Huduma ya Spotify.

Kuondoa idhini

Ondoa idhini yako inayoturuhusu kukusanya au kutumia data yako ya binafsi.

Unaweza kufanya hivi ikiwa Spotify inachakata data yako ya binafsi kwa idhini ya misingi ya kisheria.

Ili uondoe idhini yako, unaweza:

Haki ya kuwasilisha malalamiko

Wasiliana na Mamlaka ya Ulinzi wa Faragha ya nchini Uswidi au mamlaka ya ulinzi wa data ya mahali ulipo kuhusu maswali au hoja zozote.

Unaweza kupata maelezo kuhusu Mamlaka ya Uswidi hapa. Unaweza pia kwenda kwenye tovuti ya mamlaka ya ulinzi wa data ya mahali ulipo.

Vidhibiti vya matangazo yanayolenga

Matangazo yanayolengwa ni nini?

  • Hali hii ni wakati tunatumia maelezo kukuhusu kulenga matangazo ili yakufae zaidi. Hali hii inajulikana pia kama utangazaji unaolingana na mambo yanayokuvutia.
  • Mfano wa tangazo linalolenga ni pale ambapo mshirika wa utangazaji anapokuwa na maelezo yanayoonyesha kuwa unapenda magari. Maelezo haya yanaweza kutusaidia kukuonyesha matangazo kuhusu magari.

Jinsi ya kudhibiti matangazo yanayolenga:

  • Unaweza kudhibiti matangazo ya kulenga kwenye ukurasa wako wa Faragha ya Akaunti chini ya 'Matangazo ya Kulenga'.
  • Unaweza pia kudhibiti matangazo yanayolenga kwa baadhi ya podikasti ukitumia kiungo kilicho katika maelezo ya kipindi cha onyesho. Hii inatumika pale ambapo mtoa maudhui anafadhili podikasti yake kwa kuweka matangazo katika podikasti yenyewe. Vidhibiti hivi husimamiwa na mpangishaji wa podikasti, ambaye huenda asiwe Spotify.

Ikiwa 'ulijiondoa' ili usipate Matangazo ya Kulenga katika ukurasa wako wa Faragha ya Akaunti, bado huenda ukapata matangazo. Hii inaweza kuwa katika Huduma yetu Isiyolipiwa, na pia katika Huduma yetu Inayolipiwa, kama inavyotumika (kwa mfano, utangazaji katika podikasti). Aina hii ya utangazaji inatokana na maelezo yako ya kujisajili na unachosikiliza kwa sasa kwenye huduma zetu. Kwa mfano, ikiwa unasikiliza podikasti ya mapishi, unaweza kusikia tangazo kuhusu kichakataji chakula.

3. Data binafsi tunayokusanya kukuhusu

Majedwali haya yanabainisha aina za data ya binafsi tunazokusanya kutoka kwako.

Inayokusanywa unapojisajili kwenye Huduma ya Spotify
au unaposasisha akaunti yako

Aina

Maelezo

Data ya Mtumiaji

Data ya binafsi tunayohitaji ili kufungua akaunti yako ya Spotify na inayokuruhusu kutumia Huduma ya Spotify.

Aina ya data inayokusanywa na kutumiwa inategemea aina ya Chaguo la Huduma ulilonalo. Inategemea pia jinsi unavyofungua akaunti yako, nchi unakoishi na matumizi yako ya huduma za wengine kuingia katika akaunti. Hii inaweza kuwa ni pamoja na:

  • jina la wasifu
  • anwani ya barua pepe
  • nenosiri
  • nambari ya simu
  • tarehe ya kuzaliwa
  • jinsia
  • anwani ya mtaa (angalia maelezo zaidi hapa chini)
  • nchi
  • chuo kikuu/chuo (kwa Spotify Premium ya Mwanachuo)

Tunapata baadhi ya data hii kutoka kwako k.m. kutoka kwenye fomu ya kujisajili au ukurasa wa akaunti.

Pia tunakusanya baadhi ya data hii kutoka kwenye kifaa chako k.m. nchi au eneo. Kwa maelezo zaidi kuhusu jinsi tunavyokusanya na kutumia data hii, angalia 'Eneo lako la jumla (lisilo mahususi)' katika aina ya Data ya Matumizi.

Data ya Anwani ya Mtaa

Tunaweza kuomba na kuchakata anwani yako ya mtaa kwa sababu zifuatazo:

  • ili kuhakikisha umetimiza masharti ya kupata Chaguo la Huduma
  • ili kutoa ilani zinazohitajika kisheria
  • ili kutoa machaguo ya usaidizi
  • kwa usimamizi wa bili na ushuru
  • ili kukufikishia bidhaa au zawadi halisi ambazo umeagiza

Katika baadhi ya matukio, tunaweza kutumia programu ya wengine ili kukusaidia kuthibitisha anwani yako, kama vile Ramani za Google.

Yanayokusanywa kupitia matumizi yako ya Huduma ya Spotify

Aina

Maelezo

Data ya Matumizi

Data ya binafsi inayokusanywa na kuchakatwa kukuhusu unapofikia au kutumia Huduma ya Spotify.

Kuna aina chache za maelezo yanayojumuishwa katika hili, yaliyoorodheshwa katika sehemu zinazofuata.

Maelezo kuhusu matumizi yako ya Spotify

Mifano ni pamoja na:


  • maelezo kuhusu Chaguo lako la Huduma ya Spotify
  • vitendo vyako katika Huduma ya Spotify (ikiwa ni pamoja na tarehe na saa), kama vile:
    • hoja za utafutaji
    • historia ya utiririshaji
    • orodha za kucheza unazounda
    • maktaba yako
    • historia ya kuvinjari
    • mipangilio ya akaunti
    • mtagusano na watumiaji wengine wa Spotify
    • matumizi yako ya huduma, vifaa na programu za wengine yanayohusiana na Huduma ya Spotify
  • makisio (yaani, uelewa wetu) ya mambo yanayokuvutia na mapendeleo yako kulingana na matumizi yako ya Huduma ya Spotify
  • maudhui unayotoa wakati unashiriki kwenye ofa za Spotify, kama vile mashindano au bahati nasibu
  • maudhui unayochapisha kwenye sehemu yoyote ya Huduma ya Spotify. Kwa mfano: picha, sauti, maandishi, vichwa, maelezo, mawasiliano na aina nyingine ya maudhui

Data yako ya kiufundi

Mifano ni pamoja na:

  • Maelezo ya URL
  • vitambulishi vya mtandaoni kama vile data ya vidakuzi na anwani za IP
  • maelezo kuhusu vifaa unavyotumia kama vile:
    • Vitambulisho vya vifaa
    • aina ya muunganisho wa mtandao (k.m. wifi, 4G, LTE, Bluetooth)
    • mtoa huduma
    • utendaji wa mtandao na kifaa
    • aina ya kivinjari
    • lugha
    • maelezo yanayowezesha udhibiti wa haki za dijitali
    • mfumo wa uendeshaji
    • Toleo la programu ya Spotify
  • maelezo yanayotuwezesha kugundua na kuunganisha kwenye programu na vifaa vya wahusika wengine. Mifano ya maelezo haya ni jina la kifaa, vitambulishi vya kifaa, chapa na toleo. Mifano ya programu na vifaa vya wengine ni:
    • vifaa kwenye mtandao wako wa wifi (kama vile spika) ambavyo vinaweza kuunganisha kwenye Huduma ya Spotify
    • vifaa vinavyopatikana kupitia mfumo wako wa uendeshaji unapounganisha kupitia Bluetooth, programu jalizi na usakinishaji
    • Programu za washirika wa Spotify ili kubaini iwapo programu imesakinishwa kwenye kifaa chako

Eneo lako la jumla (lisilo mahususi)

Eneo lako la jumla ni pamoja na nchi, eneo au jimbo. Tunaweza kupata maelezo haya kutoka kwenye data ya kiufundi (k.m. anwani yako ya IP, mipangilio ya lugha kwenye kifaa chako) au sarafu ya malipo.

Tunahitaji maelezo haya:

  • ili kukidhi mahitaji ya kijiografia katika makubaliano yetu na wamiliki wa maudhui kwenye Huduma ya Spotify
  • ili kukupa maudhui na matangazo yanayokufaa

Data ya kihisi cha kifaa chako

Data ya kihisi cha kifaa inayotokana na mwendo au mkao ikiwa inahitajika ili kutoa vipengele vya Huduma ya Spotify vinavyohitaji data hii. Hii ni data inayokusanywa na kifaa chako kuhusu jinsi ambavyo unasogeza au kushikilia kifaa chako.

Data ya ziada unayoamua kutupatia

Aina

Maelezo

Data ya Sauti

Ikiwa vipengele vya sauti vinapatikana katika soko lako na eneo ambako umechagua kutumia kipengele cha sauti, tutakusanya na kuchakata data ya sauti. Data ya sauti inamaanisha rekodi za sauti za sauti yako na manukuu ya rekodi hizo.

Kwa maelezo zaidi kuhusu jinsi vipengele tofauti vya sauti vinavyofanya kazi, na jinsi unavyoweza kuvidhibiti na kuvizima, angalia Sera yetu ya Udhibiti wa Sauti.

Data ya Malipo na Ununuzi

Ukifanya ununuzi wowote kutoka Spotify au ukijisajili ili utumie Chaguo la Huduma inayolipiwa au ufanye jaribio, tutahitaji kuchakata data yako ya malipo.

Data mahususi ya binafsi inayokusanywa na kutumiwa itatofautiana kwa kutegemea njia ya kulipa. Itajumuisha maelezo kama vile:

  • jina
  • tarehe ya kuzaliwa
  • aina ya njia ya malipo (k.m. kadi ya mikopo au ya malipo)
  • ikiwa unatumia kadi ya malipo au ya mikopo, aina ya kadi, tarehe ya mwisho ya matumizi na tarakimu fulani za nambari ya kadi yako
    Kumbuka: Kwa usalama, huwa hatuhifadhi nambari yako kamili ya kadi
  • ZIP/msimbo wa posta
  • nambari ya simu ya mkononi
  • maelezo ya ununuzi na historia ya malipo yako

Data ya Tafiti na Utafiti

Unaposhiriki katika utafiti wa mtumiaji au kujibu tafiti, tunakusanya na kutumia data ya binafsi unayotoa.

Tunapokea baadhi ya data iliyotajwa hapo juu kutoka kwa wahusika wengine. Jedwali hapa chini linabainisha aina za wahusika hao wengine.

Vyanzo vingine ambako tunapokea data yako

Aina ya wahusika wengine

Maelezo

Aina za data

Washirika wa uthibitishaji

Ukijisajili au kuingia katika akaunti ya Huduma ya Spotify ukitumia huduma nyingine, huduma hiyo itatutumia maelezo yako. Maelezo haya yatatusaidia kufungua akaunti yako kwenye huduma zetu.

Data ya Mtumiaji

Programu, huduma na vifaa vya wengine unavyounganisha kwenye akaunti yako ya Spotify

Ukiunganisha akaunti yako ya Spotify kwenye programu, huduma au vifaa vya wengine, tunaweza kukusanya na kutumia taarifa fulani kutoka kwa mhusika huyo. Ukusanyaji huu huwezesha ujumuishaji.

Programu, huduma na vifaa hivi vya wengine vinaweza kuwa ni pamoja na:

  • mitandao ya kijamii
  • vifaa ikiwa ni pamoja na:
    • sauti (k.m. spika na vipokea sauti vya kichwani)
    • saa mahiri
    • televisheni
    • simu za mkononi na tableti
    • motokaa (k.m. magari)
    • vifaa vya michezo ya video
  • huduma au mifumo kama vile programu za kuratibu kwa sauti au mifumo ya maudhui


Tutaomba ruhusa yako kabla hatujakusanya taarifa yako kutoka kwa wahusika fulani.

Data ya Mtumiaji

Data ya Matumizi

Washirika wa huduma za kiufundi

Tunafanya kazi na washirika wa huduma za kiufundi wanaotupa data fulani. Hii ni pamoja na kuweka anwani za IP kwenye data isiyo mahususi ya mahali (k.m. nchi au eneo, jiji, jimbo).

Hii huwezesha Spotify kutoa Huduma ya Spotify, maudhui na vipengele.

Tunafanya kazi pia na watoa huduma za ulinzi wanaotusaidia kulinda akaunti za watumiaji.

Data ya Mtumiaji

Data ya Matumizi

Washirika wa malipo na Wauzaji

Ukichagua kulipa kupitia wahusika wengine (k.m. watoa huduma za simu) au kupitia ankara, huenda tukapata data kutoka kwa washirika wetu wa malipo.

Hii huturuhusu:

  • kukutumia ankara
  • kuchakata malipo yako
  • kukupa ulichonunua

Tukikuelekeza kwa muuzaji, tunapokea data kutoka kwa muuzaji huyo inayohusiana na ununuzi wako. Kwa mfano, tunaweza kukuelekeza kwenye duka la bidhaa za msanii katika mfumo wa mhusika mwingine au tovuti ya tiketi ya mhusika mwingine.

Kupokea data hii huturuhusu:

  • kukokotoa asilimia yoyote ya mauzo tunayodai
  • kuchambua ufanisi wa ushirikiano wetu na washirika hawa wa mauzo
  • kuelewa mambo yanayokuvutia

Data ya Malipo na Ununuzi

Washirika wa matangazo na masoko

Tunapokea makisio kutoka kwa washirika fulani wa utangazaji au masoko. Makisio haya ni uelewa wa washirika hawa kuhusu mambo yanayokuvutia na mapendeleo yako.

Hii hutuwezesha kutoa matangazo yanayofaa zaidi.

Data ya Matumizi

Kampuni tunazonunua

Huenda tukapokea data kukuhusu kutoka kwenye kampuni tunazonunua. Hatua hii ni kwa ajili ya kuboresha huduma, bidhaa na matoleo yetu.

Data ya Mtumiaji

Data ya Matumizi

Ukipakua programu ya vifaa vya mkononi ya Spotify na ujaribu kutumia Spotify ukiwa hujaingia katika akaunti, tutakusanya taarifa chache kuhusu matumizi yako ya Huduma ya Spotify, ikiwa ni pamoja na Data ya Matumizi. Tunafanya hivi ili kuelewa jinsi unavyofikia na kutumia Huduma yetu. Tunafanya hivi pia ili kuhakikisha tunatoa hali inayokufaa ya matumizi, kwa mfano kulingana na nchi au eneo lako. Ukiamua kufungua akaunti ya Spotify ili ufurahie huduma yetu kikamilifu, basi tutaunganisha data hii na data ya akaunti yako ya Spotify.

4. Kusudi letu la kutumia data yako ya binafsi

Jedwali lililo hapa chini linafafanua:

  • kusudi letu la kuchakata data yako ya binafsi
  • uhalali wetu wa kisheria (unaojulikana kama 'misingi ya kisheria') chini ya sheria ya ulinzi wa data, kwa kila kusudi
  • aina za data ya binafsi tunazotumia kwa kila kusudi. Angalia maelezo zaidi kuhusu aina hizi katika Sehemu ya 3 'Data ya binafsi tunayokusanya kukuhusu'

Haya ni maelezo ya jumla kuhusu kila 'misingi ya kisheria' ili kukusaidia uelewe jedwali:

  • Utekelezaji wa Mkataba: Wakati kuna umuhimu wa Spotify (au mhusika mwingine) kuchakata data yako ya binafsi ili:
    • kutii wajibu uliobainishwa katika mkataba nawe. Hii ni pamoja na wajibu wa Spotify chini ya Masharti ya Kutumia ili kukupa Huduma ya Spotify, au
    • kuthibitisha maelezo kabla mkataba mpya na wewe haujaanza kutekelezwa.
  • Maslahi Halali: Wakati Spotify au mhusika mwingine anahitaji kutumia data yako ya binafsi kwa njia fulani, ambayo ni muhimu na ina sababu mahususi ikizingatiwa hatari yoyote kwako na watumiaji wengine wa Spotify. Kwa mfano, kutumia Data ya Matumizi ili kuboresha Huduma ya Spotify kwa watumiaji wote. Wasiliana nasi ikiwa ungependa kuelewa sababu maalum.
  • Idhini: Spotify inapokuomba uonyeshe dhahiri umekubali Spotify itumie data yako binafsi kwa kusudi fulani.
  • Kutii Wajibu wa Kisheria: Wakati Spotify inapaswa kuchakata data yako ya binafsi ili kutii sheria.
Kusudi la kuchakata data yako Misingi ya kisheria inayoruhusu kusudi Aina za data ya binafsi zilizotumika kwa ajili ya kusudi

Ili kutoa Huduma ya Spotify kwa mujibu wa mkataba wetu na wewe.

Kwa mfano, tunaweza kutumia data yako ya binafsi kwa ajili ya:

  • kukufungulia akaunti
  • kuwekea akaunti yako mapendeleo, au
  • kutoa programu ya Spotify unapoipakua kwenye kifaa chako

Utekelezaji wa Mkataba

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi

Ili kutoa sehemu zaidi za Huduma ya Spotify.

Kwa mfano, tunapotumia data yako ya binafsi ili kukuwezesha kushiriki kiungo cha maudhui ya Spotify na mtu mwingine.

Maslahi Halali

Masilahi yetu halali hapa ni pamoja na:

  • kuhakikisha Huduma ya Spotify inafanya kazi na kutekelezwa ipasavyo, na
  • kuruhusu watumiaji kufikia na kutumia Huduma ya Spotify
  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi

Ili kutoa vipengele fulani vya ziada vya Huduma ya Spotify visivyo vya lazima. Tutakuomba idhini kwa uwazi iwapo hili ndilo lengo.

Idhini

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Tafiti na Utafiti
  • Data ya Malipo na Ununuzi

Ili kutambua, kutatua na kurekebisha matatizo katika Huduma ya Spotify.

Utekelezaji wa Mkataba

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi

Ili kutathimini na kutengeneza vipengele vipya, teknolojia na maboresho katika Huduma ya Spotify.

Kwa mfano:

  • tunatumia data binafsi ili kusanidi na kuboresha algoriti zetu za mapendekezo yanayokufaa
  • tunachambua jinsi watumiaji wetu wanavyochukulia kipengele fulani kipya na kuona iwapo tunapaswa kufanya mabadiliko

Maslahi Halali

Masilahi yetu halali hapa ni pamoja na kusanidi na kuboresha bidhaa na vipengele kwa ajili ya watumiaji wetu.

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Kwa matangazo au utangazaji ambapo sheria inatutaka tupate idhini yako.

Kwa mfano, tunapotumia vidakuzi kuelewa mambo yanayokuvutia au sheria inahitaji tupate idhini kwa ajili ya utangazaji kupitia barua pepe.

Idhini

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Kwa makusudi mengine ya utangazaji, ukuzaji na matangazo ambapo sheria haihitaji idhini.

Kwa mfano, tunapotumia data yako ya binafsi kufanya matangazo yakufae kulingana na mambo yanayokuvutia.

Maslahi Halali

Masilahi yetu halali hapa ni pamoja na kutumia utangazaji kufadhili Huduma ya Spotify, ili tuweze kutoa vipengele vingi bila malipo.

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Ili kutii wajibu wa kisheria ambao tunazingatia.

Hii inaweza kuwa:

  • wajibu chini ya sheria ya nchi/eneo ulipo
  • Sheria ya Uswidi (kwa sababu makao yetu makuu yapo Uswidi), au
  • Sheria ya Umoja wa Ulaya tunayoizingatia

Kwa mfano, tunapotumia tarehe yako ya kuzaliwa inapohitajika kwa ajili ya kuthibitisha umri.

Kutii wajibu wa kisheria

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Ili kutii ombi la mamlaka ya sheria, mahakama na mamlaka nyingine husika.

Kutii wajibu wa kisheria, na maslahi halali


Masilahi yetu halali hapa ni pamoja na kusaidia mamlaka ya kisheria kuzuia na kutambua uhalifu mkubwa.

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Ili kutimiza wajibu wa kimkataba na wahusika wengine.

Kwa mfano, tunapotoa data isiyomtambulisha mtu kuhusu usikilizaji wa watumiaji wetu kwa sababu tuna makubaliano ya kufanya hivyo na mmiliki wa hisa za Spotify.

Maslahi halali

Masilahi yetu halali hapa ni pamoja na:

  • kudumisha uhusiano wetu na wasanii ili tuweze kutoa Huduma ya Spotify
  • kudumisha uhusiano wetu na wahusika wengine kwa sababu hiyo hiyo
  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi

Ili kuchukua hatua zinazofaa kuhusu ripoti za ukiukaji wa hakimiliki na maudhui yasiyofaa.

Maslahi halali

Masilahi yetu halali hapa ni kulinda haki za uvumbuzi na maudhui halisi.

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi

Ili kuanzisha, kutekeleza au kutetea madai ya kisheria.

Kwa mfano, iwapo tunahusika katika kesi mahakamani na tunahitaji kuwapa mawakili wetu maelezo kuhusiana na kesi hiyo ya kisheria.

Maslahi halali

Masilahi yetu halali hapa ni pamoja na:

  • kutafuta ushauri wa kisheria
  • kujilinda sisi wenyewe, watumiaji wetu na wengine katika kesi za kisheria
  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Ili kuweka mipango ya biashara, kuripoti na kutabiri.

Kwa mfano, tunapotazama data ya watumiaji iliyojumlishwa kama vile idadi ya watu wapya waliojisajili katika nchi ili kupanga maeneo mapya ya kuzindua bidhaa na vipengele vyetu.

Maslahi Halali

Masilahi yetu halali hapa ni pamoja na kufanya utafiti na kuweka mipango ili tuendelee kuendesha biashara yetu kwa mafanikio.

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Malipo na Ununuzi

Ili kuchakata malipo yako.

Kwa mfano, tunapotumia data yako ya binafsi kukuwezesha ununue usajili wa Spotify.

Utekelezaji wa Mkataba, na idhini

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Malipo na Ununuzi
  • Data ya Anwani ya Mtaa

Ili kutunza usalama wa Huduma ya Spotify na kutambua na kuzuia ulaghai.

Kwa mfano, tunapochanganua Data ya Matumizi ili kutafuta matumizi ya ulaghai ya Huduma ya Spotify.

Maslahi Halali

Masilahi yetu halali hapa ni kulinda Huduma ya Spotify na watumiaji wetu dhidi ya ulaghai na shughuli nyingine haramu.

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Malipo na Ununuzi

Ili kufanya utafiti na tafiti.

Kwa mfano, tunapowasiliana na watumiaji wetu ili kuwaomba maoni yao.

Maslahi Halali

Masilahi yetu halali hapa ni pamoja na kuelewa zaidi kuhusu watumiaji wanachofikiri na jinsi wanavyotumia Huduma ya Spotify.

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Katika maeneo ya mamlaka ambapo maslahi halali hayatambuliki kwa misingi ya kisheria, tunategemea kigezo cha kimkataba au idhini.

5. Kushiriki data yako ya binafsi

Sehemu hii inabainisha ni nani anayepokea data ya binafsi ambayo inakusanywa au kuzalishwa kupitia matumizi yako ya Huduma ya Spotify.

Maelezo yanapokatikana kwa umma

Data ya binafsi ifuatayo daima itapatikana kwa umma kwenye Huduma ya Spotify (isipokuwa kwa mtumiaji yeyote uliyemzuia):

  • jina lako la wasifu
  • picha yako ya wasifu
  • orodha zako za kucheza za umma
  • maudhui mengine unayochapisha kwenye Huduma ya Spotify, na vichwa, maelezo na picha zozote zinazohusiana
  • unayefuatilia kwenye Huduma ya Spotify
  • anayekufuatilia kwenye Huduma ya Spotify

Wewe au mtumiaji mwingine mnaweza kushiriki maelezo fulani kwenye huduma za wahusika wengine, kama vile mitandao jamii au mifumo ya ujumbe. Hii ni pamoja na:

  • wasifu wako
  • maudhui yoyote unayochapisha kwenye Spotify na maelezo kuhusu maudhui hayo
  • orodha zako za kucheza na nyimbo, maelezo na picha zozote zinazohusiana

Data hii inaposhirikiwa, huduma ya wengine inaweza kuhifadhi nakala ili kuwezesha vipengele vyake.

Data ya binafsi unayoamua kushiriki

Tutashiriki data ya binafsi ifuatayo na walioorodheshwa katika jedwali lililo hapa chini pekee:

  • pale ambapo umechagua kutumia kipengele cha Huduma ya Spotify au programu, huduma au kifaa cha mhusika mwingine, na tunahitaji kushiriki data ya binafsi ili kuwezesha hili, au
  • ukitupa vinginevyo idhini ya kushiriki data ya binafsi. Kwa mfano, unaweza kufanya hivyo kwa kuchagua mipangilio inayofaa katika Huduma ya Spotify au kwa kutoa idhini yako
Aina za wapokeaji Sababu ya kushiriki

Programu, huduma na vifaa vya wengine unavyounganisha kwenye Akaunti yako ya Spotify

Ili kuunganisha akaunti yako ya Spotify, au ili uweze kutumia Huduma ya Spotify kuunganisha na programu, huduma au vifaa vya wengine.

Mifano ya programu, huduma na vifaa vya wengine ni kama vile:

  • programu za mitandao ya kijamii
  • vifaa vya spika
  • televisheni
  • mifumo ya motokaa
  • programu za kuratibu kwa sauti

Unaweza kuona na kuondoa miunganisho mingi ya washirika wengine chini ya 'Programu' katika akaunti yako.

Jumuiya ya usaidizi

Ili uweze kutumia huduma ya Jumuiya ya Usaidizi ya Spotify.

Unapojisajili ili kufungua akaunti kwenye Jumuiya ya Usaidizi ya Spotify, tutakuomba uweke jina la wasifu. Jina hili litaonyeshwa hadharani kwa mtu yeyote anayetumia Jumuiya ya Usaidizi ya Spotify. Tutaonyesha pia maswali au maoni yoyote utakayochapisha.

Watumiaji wengine wa Spotify

Ili ushiriki maelezo kuhusu matumizi yako ya Huduma ya Spotify na watumiaji wengine wa Spotify. Hawa wanaweza kuwa ni pamoja na wanaokufuatilia kwenye Spotify.

Kwa mfano, chini ya mipangilio ya 'Kijamii' unaweza kuchagua kushiriki wasanii uliocheza kazi zao hivi karibuni na orodha zako za kucheza kwenye wasifu wako. Unaweza pia kuchagua kuunda au kujiunga kwenye orodha ya kucheza inayoshirikiwa na watumiaji wengine. Orodha za kucheza zilizoshirikiwa hukupa mapendekezo ya kijamii kulingana na shughuli yako ya kusikiliza.

Wasanii na kampuni za kurekodi

Ili upokee habari au ofa za matangazo kutoka kwa wasanii, kampuni za kurekodi au washirika wengine.

Unaweza kuchagua kushiriki Data yako ya Mtumiaji kwa kusudi hili. Utaweza kuchagua kubadilisha mawazo yako na kuondoa idhini yako wakati wowote.

Maelezo tunayoweza kushiriki

Angalia jedwali hili la maelezo kuhusu tunayeshiriki naye na kwa nini.

Aina za wapokeaji Aina za data Sababu ya kushiriki

Watoa huduma

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Ili waweze kutoa huduma zao kwa Spotify.

Watoa huduma hawa ni pamoja na wale tunaowakodisha ili:

  • watoe usaidizi kwa wateja
  • waendeshe miundombinu ya kiufundi tunayohitaji ili kutoa Huduma ya Spotify
  • kusaidia katika kulinda mifumo na huduma zetu (k.m. reCAPTCHA ya Google)
  • kusaidia kutangaza bidhaa, huduma, matukio na ofa za Spotify (na washirika wetu)

Washirika wa malipo

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Malipo na Ununuzi

Ili waweze kuchakata malipo yako, na kwa kusudi la kuepuka ulaghai.

Washirika wa matangazo

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi

Ili waweze kutusaidia kukuonyesha matangazo yanayofaa zaidi kwenye Huduma ya Spotify na kusaidia kupima ufanisi wa matangazo.

Kwa mfano, washirika wetu wa matangazo hutusaidia kufanikisha matangazo yanayolenga.

Washirika wa Matangazo

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi

Ili kutangaza Spotify na washirika wetu. Huwa tunashiriki baadhi ya Data ya Mtumiaji na Data ya Matumizi na washirika hawa panapohitajika ili:

  • kukuwezesha ushiriki katika ofa za Spotify, ikiwa ni pamoja na majaribio au ofa nyingine zilizounganishwa
  • ili kutangaza Spotify katika maudhui na matangazo yanayochapishwa kwenye huduma nyingine za mtandaoni
  • kutusaidia sisi na washirika wetu kupima ufanisi wa ofa za Spotify

Mifano ya washirika ni pamoja na:

  • washiriki wa masoko au udhamini
  • tovuti na programu za vifaa vya mkononi zinazotuuzia nafasi ya kutangaza kwenye huduma zao
  • washirika wa kifaa, programu na vifaa vya mkononi wanaotoa pia ofa za Spotify

Washirika wetu wanaweza pia kuunganisha data ya binafsi tunayoshiriki nao na data nyingine wanayokusanya kukuhusu, k.m. matumizi yako ya huduma zao. Sisi na washirika wetu tunaweza kutumia maelezo haya kukupa ofa, matangazo au shughuli nyingine za uuzaji ambazo tunaamini zitakufaa.

Mifumo ya Kupangisha

  • Data ya Matumizi

Mifumo ya kupangisha hupangisha podikasti ili ziweze kukufikia. Tunashiriki data fulani, kama vile anwani yako ya IP, na mifumo ya kupangisha unapocheza podikasti. Tunakuruhusu pia kutiririsha podikasti zinazopatikana kwenye mifumo mingine ya kupangisha isiyomilikiwa na Spotify.

Watoa huduma za podikasti wanapaswa kufafanua katika onyesho au kipindi mfumo upi unapangisha podikasti. Angalia sera ya faragha ya mfumo wa kupangisha ili uone jinsi wanavyotumia data inayoshirikiwa nao.

Watafiti wa kitaaluma

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi

Kwa shughuli kama vile uchambuzi wa takwimu na masomo ya kitaaluma, lakini katika muundo wa utambulisho bandia pekee. Data iliyoficha utambuzi inamaanisha data inatambulishwa kwa msimbo badala ya jina lako au maelezo mengine yoyote yanayokutambulisha moja kwa moja.

Kampuni nyingine za kikundi cha Spotify, ikiwa ni pamoja na kampuni zinazonunuliwa na Spotify

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Ili kutekeleza shughuli zetu za kila siku na ili tuweze kutunza, kuboresha na kukupa Huduma ya Spotify na za kampuni tulizonunua.

Kwa mfano:

  • kuwawezesha wafanyakazi wetu wanaofanya kazi katika kampuni tofauti za kikundi kusanidi na kuboresha vipengele vya Huduma ya Spotify
  • kushiriki data na kampuni zetu za kupima ili kupima ufanisi wa kampeni za matangazo zinazoendeshwa kwenye Huduma ya Spotify
  • kushiriki data na kampuni zetu za podikasti ili kuelewa vyema zaidi mitindo ya usikilizaji wa watumiaji

Mamlaka za kisheria na mamlaka zingine, au wahusika wengine katika kesi za kisheria

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Matumizi

Wakati tunaamini kwa nia njema kuwa ni muhimu kwetu kufanya hivyo, kwa mfano:

  • ili kutii wajibu wa kisheria
  • ili kushughulikia mchakato halali wa kisheria (kama vile kibali cha utafutaji, amri ya mahakama au wito wa mahakama)
  • kwa maslahi halali ya wahusika wengine au yetu wenyewe, yanayohusiana na:
    • usalama wa taifa
    • utekelezaji wa sheria
    • kesi (kesi mahakamani)
    • uchunguzi wa kosa la jinai
    • kulinda usalama wa mtu
    • kuzuia kifo au hatari iliyopo ya kudhuru

Wanunuzi wa biashara yetu

  • Data ya Mtumiaji
  • Data ya Anwani ya Mtaa
  • Data ya Matumizi
  • Data ya Sauti
  • Data ya Malipo na Ununuzi
  • Data ya Tafiti na Utafiti

Iwapo tungeuza au tungejadiliana kuuza biashara yetu kwa mnunuzi au mnunuzi mtarajiwa.

Katika hali hii, tunaweza kuhamishia data yako ya binafsi kwa mrithi au mshirika kama sehemu ya mchakato huo.

6. Uhifadhi wa data

Tunahifadhi data yako ya binafsi kadri tunavyoihitaji ili kukupa Huduma ya Spotify na kwa makusudi halali ya Spotify na michakato muhimu ya biashara, kama vile:

  • kudumisha utendaji wa Huduma ya Spotify
  • kufanya maamuzi ya biashara yanayotokana na data kuhusu ofa na vipengele vipya
  • kutii wajibu wetu wa kisheria
  • kutatua migogoro

Hizi ni baadhi ya aina za vipindi vyetu vya kuhifadhi, na vigezo tunavyotumia kuvibainisha:

  • Data inayohifadhiwa hadi utakapoiondoa
    Ni haki yako kuomba tufute baadhi ya data yako ya binafsi. Angalia sehemu ya 'Kufuta' katika Sehemu ya 2 ya 'Udhibiti na haki zako juu ya data yako ya binafsi' kwa maelezo zaidi, na hali ambapo tunaweza kutekeleza ombi lako.
    Unaweza pia kufuta data fulani ya binafsi moja kwa moja kwenye Huduma ya Spotify: kwa mfano, unaweza kubadilisha au kufuta picha yako ya wasifu. Pale ambapo watumiaji wanaweza kuona na kusasisha wenyewe data ya binafsi, tunahifadhi maelezo kwa muda ambao mtumiaji atakaochagua isipokuwa pale ambapo mojawapo ya madhumumi machache yaliyofafanuliwa hapa chini yanatumika.
  • Data ambayo muda wake wa kutumika huisha baada ya muda mahususi
    Tumeweka vipindi fulani vya kuhifadhi ili muda wa kutumia baadhi ya data uishe baada ya kipindi mahususi. Kwa mfano, data ya binafsi unayoweka kama sehemu ya hoja za utafutaji hufutwa kwa ujumla baada ya siku 90.
  • Data inayohifadhiwa hadi akaunti yako ya Spotify itakapofutwa
    Tunahifadhi data fulani hadi utakapofuta akaunti yako ya Spotify. Mifano ya data hii ni pamoja na jina la mtumiaji na maelezo ya wasifu wako kwenye Spotify. Kwa kawaida huwa pia tunahifadhi historia ya utiririshaji kwa kipindi chote unachotumia akaunti, kwa mfano, ili kutumia data hii kutoa orodha za kucheza ambazo watumiaji wanafurahia na mapendekezo yaliyowekewa mapendeleo yanayozingatia taratibu za usikilizaji (kwa mfano, Burudani Yako Inayofaa Nyakati Zote au Mseto Wako wa Sikukuu). Unapofuta akaunti yako ya Spotify, aina hii ya data hufutwa au kubadilishwa ili isikutambulishe.
  • Data inayohifadhiwa kwa vipindi virefu vya muda kwa madhumuni machache
    Baada ya akaunti yako kufutwa, tunahifadhi baadhi ya data kwa kipindi kirefu zaidi lakini kwa madhumuni machache sana. Kwa mfano, tunaweza kuhitajika kisheria au kimkataba kufanya hivi. Hii inaweza kuwa ni pamoja na sheria za lazima za uhifadhi wa data, maagizo ya serikali ya kuhifadhi data inayohusika katika uchunguzi, au data inayohifadhiwa kwa madhumuni ya kesi mahakamani. Huenda tukahifadhi data ambayo imeondolewa kwenye Huduma ya Spotify kwa kipindi kifupi. Hii inaweza kuwa:
    • kusaidia kuhakikisha usalama wa mtumiaji, au
    • kulinda dhidi ya maudhui hatarishi kwenye mfumo wetu.

Hatua hii inaweza kutusaidia kuchunguza ukiukaji unaoshukiwa wa Miongozo yetu ya Watumiaji na Kanuni za Mfumo. Kwa upande mwingine, tutaondoa maudhui yasiyo halali iwapo sheria itatuhitaji kufanya hivyo.

7. Kuhamishia nchi zingine

Kwa sababu ya hali ya kimataifa ya biashara yetu, Spotify hushiriki data ya binafsi kimataifa na kampuni za Spotify, wakandarasi wadogo na washirika ili kukupa Huduma ya Spotify. Wanaweza kuchakata data yako katika nchi ambako sheria zake za ulinzi wa data hazichukuliwi kuwa ni thabiti kama zilivyo sheria za Umoja wa Ulaya au sheria zinazotumika unakoishi. Kwa mfano, huenda wasikupe haki sawa kuhusu data yako.

Kila tunapohamisha data ya binafsi kimataifa, tunatumia zana:

  • kuhakikisha uhamishaji wa data unatii sheria inayotumika
  • kusaidia kuipa data yako kiwango sawa cha ulinzi kama ilivyo katika Umoja wa Ulaya

Ili kuhakikisha kila utumaji wa data unatii sheria zinazotumika katika Umoja wa Ulaya, tunatumia mbinu za kisheria zifuatazo:

  • Vifungu vya Kawaida vya Mikataba ('SCCs'). Vifungu hivi vinahitaji mhusika mwingine alinde data yako na akupe ulinzi na haki za kiwango cha Umoja wa Ulaya. Kwa mfano, tunatumia SCC kuhamisha data ya binafsi iliyofafanuliwa katika Sehemu ya 3 'Data ya binafsi tunayokusanya kukuhusu' kwenda kwa watoa huduma wetu wa kupangisha wanaotumia seva zao zilizo Marekani. Unaweza kutekeleza haki zako chini ya Vifungu vya Kawaida vya Mikataba kwa kuwasiliana nasi au mhusika mwingine anayechakata data yako ya binafsi.
  • Maamuzi ya Kutosheleza. Hii inamaanisha kuwa tunatuma data ya binafsi katika nchi zilizo nje ya Eneo la Kiuchumi la Ulaya ambazo zina sheria zinazojitosheleza za kulinda data ya binafsi, kama inavyofafanuliwa na Tume ya Ulaya. Kwa mfano, tunatuma data ya binafsi iliyofafanuliwa katika Sehemu ya 3 'Data ya binafsi tunayokusanya ' kwa washirika walio nchini Uingereza, Kanada, Japani, Jamhuri ya Korea na Uswisi.

Tunatambua pia na kutumia ulinzi wa ziada kama unavyohitajika kwa kila uhamishaji wa data. Kwa mfano, tunatumia:

  • ulinzi wa kiufundi, kama vile usimbaji fiche na utambulisho bandia
  • sera au michakato ya kupinga maombi ya mamlaka ya serikali yasiyo na uwiano au yaliyo kinyume cha sheria

8. Kutunza usalama wa data yako ya binafsi

Tumejitolea kulinda data ya binafsi ya watumiaji wetu. Tumeweka hatua zinazofaa za kiufundi na mipango ili kulinda usalama wa data yako ya binafsi. Hata hivyo, fahamu kuwa hamna mfumo ambao ni salama kabisa daima.

Tumetekeleza mbinu mbalimbali za kulinda dhidi ya ufikiaji usioidhinishwa na uhifadhi usiohitajika wa data ya binafsi kwenye mifumo yetu. Hizi ni pamoja na utambulisho bandia, usimbaji fiche, ufikiaji na sera za uhifadhi.

Ili kulinda akaunti yako ya mtumiaji, tunakuhimiza:

  • tumia nenosiri thabiti ambalo unatumia tu kwenye akaunti yako ya Spotify
  • usiwahi kushiriki nenosiri lako na mtu yeyote
  • dhibiti ufikiaji wa kompyuta na kivinjari chako
  • ondoka katika akaunti mara tu unapomaliza kutumia Huduma ya Spotify kwenye kifaa kinachoshirikiwa
  • soma maelezo zaidi kuhusu kulinda akaunti yako

Unaweza kuondoka katika akaunti ya Spotify kwenye maeneo mengi kwa wakati mmoja kwa kutumia kipengele cha 'Ondoka katika akaunti kila mahali' kwenye ukurasa wa akaunti yako.

Ikiwa watu wengine wana idhini ya kufikia akaunti yako ya Spotify, basi wanaweza kufikia data yako ya binafsi, vidhibiti na Huduma ya Spotify inayopatikana kwenye akaunti yako. Kwa mfano, huenda ulimruhusu mtu kutumia akaunti yako kwenye kifaa kinachoshirikiwa.

Ni wajibu wako kuwapa ruhusa tu watu ambao huna wasiwasi kushiriki nao data hii ya binafsi ili wafikie akaunti yako. Matumizi ya akaunti yako ya Spotify na mtu mwingine yeyote kunaweza kuathiri mapendekezo yako ya binafsi na kujumuishwa katika data yako unayopakua.

9. Watoto

Kumbuka: Sera hii haitumiki kwenye Spotify ya Watoto isipokuwa Sera ya Faragha ya Spotify ya Watoto iseme hivyo. Spotify ya Watoto ni programu tofauti ya Spotify.

Huduma ya Spotify ina kiwango cha chini cha 'Kikomo cha Umri' katika kila nchi au eneo. Huduma ya Spotify hailengi watoto ambao umri wao:

  • ni chini ya umri wa miaka 13, au
  • unafanya kuwa haramu kuchakata data yao ya binafsi, au
  • unahitaji idhini ya mzazi ili kuchakata data yao ya binafsi

Hatukusanyi au kutumia kwa makusudi data ya binafsi kutoka kwa watoto walio chini ya Kikomo cha Umri kinachoruhusiwa. Ikiwa uko chini ya Kikomo cha Umri, usitumie Huduma ya Spotify, na usitupe data yoyote ya binafsi. Badala yake, tunapendekeza utumie akaunti ya Spotify ya Watoto.

Ikiwa wewe ni mzazi wa mtoto aliye na umri wa chini ya Kikomo cha Umri na umegundua mtoto wako ametoa data ya binafsi kwa Spotify, wasiliana nasi.

Tukigundua kuwa tumekusanya data ya binafsi ya mtoto aliye na umri wa chini ya Kikomo cha Umri, tutachukua hatua zinazofaa kufuta data hiyo ya binafsi. Hatua hii inaweza kutuhitaji kufuta akaunti ya Spotify ya mtoto huyo.

Unapotumia kifaa kinachoshikiriwa kwenye Huduma kuu ya Spotify, kuwa mwangalifu kuhusu kucheza au kupendekeza maudhui yoyote kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 18 ambayo huenda yasiwafae.

10. Mabadiliko ya Sera hii

Huenda tukafanya mabadiliko katika Sera hii mara kwa mara.

Tunapofanya mabadiliko ya msingi kwenye Sera hii, tutakupa ilani dhahiri kama inavyotupasa kufanya katika hali hiyo. Kwa mfano, tunaweza kuonyesha ilani dhahiri ndani ya Huduma ya Spotify au kukutumia barua pepe au arifa kwenye kifaa.

11. Jinsi ya kuwasiliana nasi

Kwa maswali au hoja zozote kuhusu sera hii, wasiliana na Afisa wetu wa Ulinzi wa Data kupitia mojawapo ya njia hizi:

  • barua pepe privacy@spotify.com
  • tuandikie kupitia: Spotify AB, Regeringsgatan 19, 111 53 Stockholm, Uswidi

Spotify AB ndiye mdhibiti wa data ya binafsi inayochakatwa chini ya Sera hii.

© Spotify AB